TUENDELEE
Ninakumbuka kipindi niko shuleni, hasa katika wakati wa michezo pale wanafunzi wenzangu na mimi tulipokuwa tukiweka miili yetu sawa kiafya kwa kukimbia na kucheza mpira. Lakini jambo ninalo likumbuka sana ni wakati ule ambapo,niliujua mchezo wa mbio za  kupeana vijiti .Mantiki yake ina umaridadi mkubwa katika dhana ya umoja hasa pale washindani mnapokuwa ‘’fiti’’. Kwa hali ya sasa, wakati huu, dakika hii ninapoandika makala hii Februari 13 mwaka 2016, ni miezi miwili tu imepita tangu tufanye uchaguzi na kuaga mwaka 2015. Yaliojiri mwaka jana yamebaki mwaka jana sasa ni kuendelea  na kazi, na kwa vile dhamira ya kiongozi wa juu wa nchi yetu ni ‘’ Kazi Tu!’’  basi kijiti changu kimepewa mimi mwingine mwenye mwili wa nyama uleule lakini mwenye nia, ari na morali zaidi.

Tangia nifahamu juu ya tarehe mosi ya kila Januari, na usiku wa kuieleta kwake nimekuwa nikiwaza sana kauli mbalimbali za watu wanaonizunguka juu ya upeo wao, pale wanaposema ‘ ‘ huu ni mwaka mpya ’’. kwa akili ya kawaida kwa binadamu mwenye kuweka dhana kama hii katika hali ya asili katika tafsiri ya haraka haraka ni kama hivi; mwaka mpya ni kitu ambacho kila muda muafaka ukifika vitu vinavyo akisi umaana wake vinabadilika na kuwa upya, miezi siku majira, na tarehe. Huu mtazamo upo ndani ya watoto wengi, na ulikuwa ndani yangu wakati nilipokuwa bado mtoto, na katika hali ambayo kwa kweli si ya kawaida kwa hali niliyo nayo sasa kila kulipokuwa kukikucha na kuikaribisha asubuhi ya tarehe Mosi, kwangu ilikuwa ni siku tofauti licha ya kwamba hali ya hewa, mazingira, watu na nafsi yangu vyote vilikuwa vilevile. Na kikubwa nilichokuja gundua ni kwamba si kuuona Mwendelezo, upya ulitawala.

Dunia inaendelea na mambo yake, IS bado wanatawala sehemu mbalimbali Syria na Libya wakisambaza hofu kwa watu, nchi za ulaya bado zinapokea wakimbizi toka Syria, Africa Magharibi,Libya Na yemen, wanaowapokea bado wanajadiliana ni njia ipi watumie kuwakwepa, wajerumani bado wanaendelea kujitahidi wastiri japo kuwa wajerumani wenzao pia hawawataki kabisa wageni. Licha ya kuwa tarehe zinabadilika na kutuletea miaka, mambo yetu hayabadiliki, mwaka  mpya una ashiria kuwa ; muda wako ulipewa katika kipindi husika umekwisha, muda zaidi umewadia , Je? Tasmini yako ya mambo uliyoyafanya kwa mwaka mzima ina mashiko sanjari na hilo ,endelea na mambo yako  kwa muda huu wa nyongeza uliopewa na asili. Kwa upeo wangu nafikiri mwaka mpya uliitwa ‘’Mwaka Mpya ’’ kwa sababu ; mwongozo wa muda, siku  na majira unao tafsiriwa na kalenda ya mwaka husika umefikia kikomo na kalenda mpya inawadia, na dhahiri ina maanisha kuwa mwaka umekwisha,  na mfumo mpya(kalenda) wa siku kwa wanadamu umewadia. Kuwa dhahiri kidogo kwa sasa Tanzania na Dunia kwa ujumla ina utumia mfumo wa kalenda ya Gregory iliyoanza kutumika mnamo mwaka 1582.

Kwa wanadamu kila siku inakuja na mambo mapya na fursa mbalimbali za kutumia, kwa werevu wanazitumia vilivyo kama vile hawataiona kesho, na wakifanikiwa kuiona kesho na kwa bahati nzuri kesho hiyo ikaangukia Tarehe Mosi  ya Mwaka Mpya, nina uhakika hawata kuwa na budi kuendelea na jitihada zao za kujipatia Riziki. Mwalimu na mwanafunzi mwaka mpya unawapa wote Jua, Mwanga Wa mwezi, Usiku na Mchana namna wanavyotumia nafasi hizo ni juu yao, jambo la msingi ni kuacha dhana ya kuweka mambo mapya mbele kila mwaka mpya unapofika wakati ya kale bado hayaja maliziwa na wakati mwingine hata kufanyiwa kazi. Kuendelea pale ulipoacha ni jambo linaloonyesha kuwa unajali, na umehamasika na kile unacho kifanya cha msingi ni kujitahidi kumaliza kwa heri na fanaka. Maana kila mwaka unakuja na mambo yake. Ukweli ni kwamba mwaka mpya unafaida kwa watu walio katika mrengowa kushoto kwa namna moja au nyingine, maana nimeshuhudia watu wakiweka nadhiri kuacha mambo maovu, dhambi, na kuwa wapya na kujisafisha nafsi zao yote hayo ni kuhakikisha Mwaka mpya unapokelewa kwa heri na watu safi, wanaondelea kuishi lakini wakiishi kwa mrengo na fikra mpya.


Tuendelee na jitihada za kuifanya nchi yetu Tanzania kuwa nchi yenye amani na umoja, utawala wa sheria uimarike, haki na uhuru wa kila raia kuheshimiwa, na chini ya uongozi wa Dk. John Magufuli nchi yetu ing’are katika sekta nyeti; Elimu,afya na uchumi. Licha ya kuwa Rais wetu kaapishwa mwaka jana, juhudi na kazi zake zinaendelea, mwaka mpya umempa nafasi ya kuona hali ya nchi na kupata muda wa ziada kuendelea itengeneza nchi na kwa ushirikiano wetu watanzania tutafika tunapopataka, tusome vitabu, kwa maarifa na kufikiri zaidi. Tuendelee.

Comments