JAMII ISIYOFIKIRI KWA KINA NI HATARI

  

Padili James Mikomangwa

 


Imekuwa desturi kwa wanadamu kunyambua kila jambo linaloletwa mbele yao, tokea kuanzishwa kwa misingi ya dunia kuchanganua mambo kwa kina imekua tabia yetu. Tumeona kwa mifano mingi hai kwa watu wanaoweza kufikiri  kwa weledi(ulimwenguni kote) hujikuta wakifanikiwa katika kila nyanja ya maisha na wale wanaofanya kinyume cha hapo mara nyingi mwisho wao huwa si mzuri sana kusimulia hata ikiwa kama hadithi kama ile ya mzee tola.

Si jambo la kubeza wala kuongelea sana kwa vile lulu za fikra pevu huokoa zaidi kuliko ndimi zinazo nena sana. Je? Jamii zetu ziko katika uwanja upi wa fikra ?, ni ule wenye fikra pevu zinaweza ongelea mambo magumu na kuyapatia maelezo makini na si majibu rahisi au ule uwanja wa wachezaji wengi wasio na ujuzi wa kufikiri?.

Yamkini kufikiri kunaweza kuwa na tafsiriwa tofauti sana na watu wa haiba kadha wa kadha , ili kuweka mambo sawa tunaweza sema: kufikiri ni hatua inayochukuliwa na mwanadamu mwenye akili timamu inayohusisha kunyambua mambo mbalimbali yenye utata na kinzani , pima mantiki katika hoja , angalia umuhimu wa mambo kwa jicho makini zaidi ya lile la nyama na kupata hitimisho lililosheheni maamuzi chanya  na yakinifu.

Mara nyingi kufikiri kunahitaji muda, utulivu wa nafsi, mwili na akili yako kwa ujumla. Ni nadra sana kukuta maamuzi chanya yanachukuliwa pale mtu anapofikiri kwa pupa na akiwa na mihemuko, kwa vile akili zetu huzidiwa na mihemuko inayochukua sehemu ya ubongo wenye uwezo wa kutambua mambo kwa weledi.

Jamii zetu zimekuwa na mabadiliko makubwa sana ya kitamaduni, kiteknolojia, kisiasa na katika Nyanja mbalimbali za kimaisha zinazopatikana katika nchi za ukanda wa chini ya jangwa la sahara kama Tanzania. Lakini kabla ya kwenda mbali zaidi, jamii ni nini hasa?.

 Tunaweza kusema jamii ni muunganiko wa watu wanaoishi katika eneo Fulani la kijiografia wenye tamaduni, mila, desturi, historia, lugha moja inayowaunganisha na mifumo ya uchumi. Katika taifa linalokua kiuchumi lenye watu zaidi ya million 50, jamii zake zitakuwa na mchanganyiko wa mambo kadha wa kadha hasa hasa tamaduni , mila na desturi zinazounda utu wa watu.

Tangia kupata uhuru tumekuwa na mabadiliko chanya katika ulingo wa maendeleo, ambapo tumeona na tunazidi shuhudia teknolojia ikichukua hatamu katika kubadili maisha yetu. Wimbi kubwa limekuwa la vijana wanaobadili namna maisha yanavyoendeshwa, na hi inatokana na uwezo mkubwa wa vijana wa karne ya 21 kujihuisha kirahisi na mabadiliko ya teknolojia pevu duniani inayochegeza ubadilishwaji wa maisha yetu ya kale na yaliyopitwa na wakati (yakiwa maoni ya wakosoaji baadhi) na kuangalia maisha mapya ya dunia kiganjani na utumiaji wa mitambo imara kufanya kazi ambazo zilifanya na binadamu kupunguza nguvu kazi ambayo haipati mbadala, yote hayo ni kuokoa muda na gharama za uzalishaji.

Siwezi elezea kwa maneno mengi juu ya jamii zetu lakini kwa mtu mwenye nia ya dhati na chachu ya maendeleo ya kweli, atajua kuwa kwa miongo 3 iliyopita kumekuwa na tofauti kubwa sana kwa watu hasa hasa pale wanapotakiwa kunyambua mambo nyeti , rahisi, yenye kuzua hisia na hata pumba kwa weledi.

Tumekuwa tukiona mihemuko ikichukua hatamu pale porojo za siasa zinapoingia na kuchukuliwa kama mantiki, kelele zisizo na msingi kuandikwa kama hoja na watu tuliowaamini kutupa habari za kina kila kukicha, tunashuhudia pale hoja za uchumi, elimu na habari za kutatanisha zinapo ibua mijadala isiyoleta suluhisho endelevu. Haya yote yanatokea mbele ya macho yetu na ni matokeo ya jamii kulaza akili na kuwaachia watu wachache wasio na ujuzi wa kunyambua hoja nyeti jukumu la kufikiri kwa niaba yetu.
Wakati nakua sikuwahi kuona wana jamii wenzangu waki payuka maneno yasio na msingi juu ya hoja waliyosikia tena kupitia mtu baki au chanzo chochote cha habari ukilinganisha na sasa, nakumbuka walisisimuka kama wengine (ni asili ya binadamu pale mambo yanayotuhusu yakihusika) lakini walikaa wakatuliza vichwa na kuanika hoja mezani kujaribu kudadavua kabla ya kuhukumu.

 Mtiririko huu ni muhimu sana kwa mtu yeyote kuufuata maana utaokoa nguvu, maumivu na majuto mengi (sote tunajua hasara ya kinyume na hili) lakini kwa karne hii yenye utandawazi, teknohama makini na ujuzi wa habari kwa haraka sana inashindwa tekeleza kazi hii ndogo. Inashangaza sana  na mbaya zaidi kuto kuhimili misingi hii ya fikra kunagharimu sana kushinda tunavyoweza fikiri. Ikumbukwe kuwa si kila msomi au mtu mwenye ujuzi wa mambo mengi anaweza kuwa na weledi wakufikiri kwa kina, kwa sababu kufikiri kwa kina kunahitaji utulivu na uwezo wa kuweka mambo bayana, na kuona vitu katika pande zote jambo ambalo si kila mtu anaweza fanya kirahisi, hata kama ni mhitimu wa elimu ya juu.

Wana jamii wanapoweza kujenga misingi na tamaduni ya kufikiri kwa kina ni vigumu sana kwa hoja za kijuha, pumba, uzushi na kelele za watu walio shika hatamu katika ngazi mbali mbali kwenye jamii kusambaza hoja zao zisizo na mashiko zilizo undwa kusambaratisha umoja wetu na mshikamano tuliojenga kwa nguvu kubwa. Jamii zetu zinaundwa na watu wa rika mbali mbali, wenye tofauti  za kichumi, elimu, maoni ya kisiasa, imani na tamaduni. Kitu cha kujivunia juu ya Tanzania yetu ni kwamba tumekuwa tukiheshimu tofauti hizi baina yetu kwa muda mrefu sasa, lakini  tokea mitandao ya kijamii ilipochukua nafasi ya kujamiana iliyokuwepo kabla, tumedhihirisha kabisa kuwa teknolojia inabadili namna akili zetu zinavyofikiri hasa  kwa sasa ambapo kuna wimbi kubwa la hoja tata zinazojadiliwa na watu wasio na weledi wa kufikiri kwa kina ambao tunawapa jukumu kubwa kama ‘’ wachambuzi wa mambo mtambuka yanayohusu Tanzania hasa siasa’’.

Hakuna jambo lolote ambalo linaweza katiza mbele yetu lisilo na mashiko kwetu na kwa kizazi kitakachofuata likakubalika kirahisi endapo tuta ichukua misingi ya fikra pevu na kuithamini kama tunavyojithamini sisi na simu zetu za mkononi. Hatari ya kutofikiri kwa kina kama jamii hujongea pale mambo muhimu sana yanapo jadiliwa kwa namna rahisi, isiyo jenga na kupelekea kufanya kwa maamuzi yasiyokuwa endelevu kwa manufaa ya jamii na kizazi kijacho.

Tuna shuhudia sasa namna masuala ya huduma za kijamii kama vile afya na elimu kwa kuanzia yanawekwa kando na mkumbo wa siasa ukichukua hatamu. Hata kama tukiyajadili hatu fanikiwi kupata upembuzi yakinifu na kupata mipango yakinifu na hata ile sehemu kubwa ya watu wenye ushawishi na wanaotegemewa kubadili akili za watu ( na inashangaza kwa jamii yetu kuwapa vinara wa mitandao ya kijamii nafasi nyeti sana) ndani ya jamii haifainikiwi kutatua mambo haya.

Sio kwamba hakuna kabisa watu wenye uwezo wa kufikiri kwa kina, watu hawa wapo ndani ya familia zetu huenda wakawa ni wenzi, wazazi, watoto , kaka hata dada ambao hawasikilizwi kwa kina kama vinara wa migomo mavyuoni na waandishi wa taarifa zisizo na mashiko mitandaoni kila kukicha.

Kwa muda sasa kama taifa tumeacha kusoma vitabu na maandiko mbalimbali kujijazia maarifa kwa muda mrefu licha ya kwamba teknolojia ina rahisisha upatikanaji wa taarifa lakini hatuna taarifa za muhimu. Nashindwa kuelewa ni wapi tulipojisahau ambapo tukaziacha njia kuu zenye kutupeleka katika maarifa yanayotuongoza katika maisha, yamkini mabadiliko ya maisha ya mwanadamu au hali ya kiuchumi, hali ya yote ulinzi wa vichwa vyetu ni muhimu sana kuliko kitu chocote maana akili inayofikiri japo kidogo haiwezi tekwa na maneno ya watu yasiyo na umuhimu.

Naona ni muhimu sana kuanza wajenga vijana wetu na watoto jinsi ya kufikiri na kujua kuchambua kati ya mantiki na upuuzi, kauli tata na kauli za kijuha, ukweli na uongo,  pamoja na hadithi za kila siku zinazo andikwa na watu mashuhuri wasio na ujuzi wa kufikiri. Kwa sasa tunapokea mambo mengi sana yanayoingia toka nchi za nje ya bara la Afrika na Tanzania kwa ujumla ,kwa hiyo si jambo rahisi na ikumbukwe kuna vita vya kiuchumi na kielimu ambavyo vinatekelezwa kwa weledi mkubwa sana (wengi wetu hatujui) na kama jamii zetu ziko gizani tutegemee majanga makubwa sana yatakayo tugharimu utu wetu na uhuru wa kufikiri kwa vizazi na vizazi.

Ni hatari sana kwa jamii, pale inapojulikana kuwa haina uwezo mkubwa wa kuchambua mambo, kwa sababu yeyote mwenye uwezo wa kukamata hisia na akili za watu anaweza penyeza lolote kwa jamii na kuivuruga vuruga kabisa. Haya yanaonekana wakati wa shughuli za kisiasa, shughuli za kiimani, sherehe na  mikumbo isiyokuwa endelevu ni ishara ya jinsi watu wetu wanavyofuata hisia za watu wachache wenye ushawishi. Dunia tunayoishi haina huruma kwa roho isiyo na akili inayoweza pembua hoja, tutaburuzwa na wanaojua kufikiri mpaka kiama, kama tukianza jiimarisha katika nyaja hii tutakuwa hatari na hakuna wa kutubabahisha kamwe.

Kwa sasa ni nadra sana kwa wale wenye elimu na nafasi ya kusema kupitia mitandao ya kijamii, kuwaona wakitetea haki za wanyonge na wasio na uwezo wa kufikisha vilio vyao. Ni watu wachache sana (pongezi kwao) wanaotekeleza jukumu hili, bahati mbaya hawapati nafasi ya kupanuka kwa sababu maisha ya watu mashuhuri ni muhimu sana kuliko kuzijua takwimu za kiuchumi, kujadili soka ni lulu kwetu kuliko kutatua adha za maji kama wanajamii na si mashabiki wa siasa.


Vita vya dhidi ya akili zetu na uhuru wa kufikiri vipo hai na vinazidi pamba moto, wengi wetu hatujui kama vita hivi ni kweli au la, lakini nipende kukuhakikishia kuwa  ni vita hatari kushinda tunavyo weza fikiri, maana hakuna watu hatari kama wafu waishio na hakuna watu hatari zaidi kwa maadui zetu wa fikra kama  wanajamii wenye uwezo mkubwa wa kufikiri. Kwa kweli tumechelewa sana kimaendeleo ukilinganisha na tuliokuwa nao sawa miaka 50 iliyopita ndugu zetu Wachina na Korea. Hatuwezi fika huko bila kuanzia tengeza mbinu za kufikiri kwa kina sasa. Kumbuka mteja wa mambo yaliyotokana na fikra pevu za wengine(ambazo si zetu wa Tanzania/Afrika) ni sisi, na kamwe wanaotupatia mambo haya hawatoruhusu sisi(Wateja) kufunguka kamwe. Hebu sasa tufunguke.

Comments