Ni nia ya dhati
inayowafanya watu katika jamii husika kufikia malengo yao na ni mipango
madhubuti inayofanikisha malengo hayo, lakini kama mipango haina uhai ndani
yake sidhani kama malengo yatafikiwa. Kama watu weusi wanaoishi marekani( kaka
, dada, mama na baba zetu) wanaweza kutoa sadaka ya dola za kimarekani millioni
252 (takwimu zilizokusanya na watafiti huru) kwa kila jumapili sawa na
zaidi ya billioni 568 za kitanzania na ili hali hawana hata mabenki yao, shule
zao wenyewe, hospitali, taasisi za kifedha , mifumo ya usambaji na viwanda hali
kadhalika na uwekezaji madhubuti. Hebu fikiria jumla ya billioni 14 za
kimarekani ambazo ni ma trillioni ya kitanzania yanatumika kama sadaka na fungu
la kumi, wakati wanategemea huruma ya weupe kupata mahitaji yao ikiwa ni zaidi
ya asilimia 40 ya watu weusi. Kuna haja ya kuwa na kanisa lenye utajiri wa mabilioni wakati waumini
wake hawawezi hata jihudumia kikamilifu? Je Malengo ya millenia yatafikiwa kweli?
Pesa inayochumwa na mtu
si haki yangu kuiongelea ila kama hata senti moja ya mtu/watu fulani inatumika
katika mfumo usio na manufaa na senti hiyo itaweza okoa nafsi za wengi, nina amini kuna
haja ya kuisemea. Sina kipingamizi na hili suala la kumtolea Bwana ila je ? Tunatumia
rasilimali zetu tulizonazo kwa umakini maana kama tunaweza toa pesa nyingi
hivi( nikimaanisha waafrika walioko nje ambao ni sawa na sisi ukiwa na mrengo
wa afrika moja) kwa ajili ya kuabudu tu na si kingine ,hakuna haja ya kulaumu
juu ya maswahibu ya kiuchumi yanayotukabili, ikiwemo kuachwa kiuchumi , kiteknolojia na
katika nyanja lukuki na wenzetu wachina pamoja na wazungu waliotutawala na wanaoendelea
kututawala bila pingu wa kengele.
Hii inadhihirika hata
kwetu huku (Kusini mwa jangwa la Sahara), naamini tuna uwezo mkubwa wa kufanya
mengi zaidi tukifungua macho na kuona namna rasilimali zetu zinavyoweza kufanya
kazi zaidi ya vile tunavyoweza fikiri. Takwimu zilizofanya na Pew survey (2010)
ilionyesha kuwa asilimia 61.4 ya watanzania kuwa ni waumini wa dini ya kikristo,
na asilimia zilizobaki kugawanyika kwa imani zingine, kwa namba zinavyo onyesha
idadi kubwa ya watu ni wakristo ambao mafunzo ya dini yana wasihi kuwa watoaji
wazuri, je? hatuwezi geuza mshale huu na kuangazia duru za kimaendeleo?
Hebu tuangalie pesa
zinazotolewa katika sherehe mbalimbali, hafla zisizo na msingi katika jamii
zetu, zingeweza fanya mambo mengi sana katika jamii kama mtu mmoja mmoja
angejikita japo kwa nafasi aliyonayo kuwa katika wimbi linalo chegeza na kuleta
mabadiliko, katika afya, usambazi wa huduma nyeti kwa jamii, elimu kwa watoto na watu wazima, kuwasaidia wasiojiweza, ulinzi wa raia na mali zao na ushirikiano wa pamoja.
Si vibaya kuabudu, sina
hila na imani yeyote ile ( unaweza abudu chochote ) ila utaifa kwanza, tofauti
zetu za kiimani, kikabila na kiitikadi zikae pembeni pale masuala ya taifa
yanapohitaji umakini wetu wa kuyanyambua hoja tata kwa weledi.
Bado sisi pamoja na
ndugu zetu walioko Marekani tuko kwenye lindi la umasikini, ili hali tuna
mtolea Mungu sadaka na zaka nyingi kushinda weupe (waliotutawala na
waliotuletea hizi dini tunazozo shabikia kila leo) ambao wanazidi kuchochea
upofu wetu katika mambo ya msingi. Tuna wachungaji matajiri sana kibao, wakati wajasiria mali waliowekeza kwenye kiini cha uchumi wachache
sana, japo wapo wengi wanajitahidi kujitanua katika uwekezaji nawapongeza. Lakini bado hatuwezi lilia
demokrasia, uhuru wa kuongea( kama vile haupo ) na propaganda zingine wakati
bado mambo nyeti kama haya hatuyatilii maanani kabisa. Ni Afrika na ni waafrika pekee ambao wanaweza kuabudu siku nzima hata kila siku ndani ya wiki, bila kupata maarifa/ujuzi wowote wa kutumia baada ya ibada katika dunia halisi ya ubepari. Kwa kweli sijawahi ona wala sikia mahubiri ambayo
yanawa sihi waafrika kusimama imara na kuushinda ubepari wa mtu mweupe kwa kutumia mbinu za kidunia zenye msingi wa kiimani.
Miaka inakwenda na bado
tunashikilia taratibu zile zile katika kuabudu ambazo bado hazitupeleki katika
hatua za juu katika nyanja za maendeleo, laiti kama makanisa yetu yangekuwa
yanatumika kama chombo cha kuwa andaa vijana kikamilifu kuivaa dunia hii
isiyokuwa huruma kwa wanyonge na wasiokuwa na maarifa naamini lindi la
umasikini lingekuwa chini. Kama tunaweza fanya harambee za kujenga makanisa
makubwa (mahekalu) yenye vito vya thamani, iweje tushindwe (kwa kanisa moja
moja) wasomesha vijana wetu wenye vipawa mbali mbali katika vyuo ili kupata
maarifa na kuisaidia jamii/taifa kupanua kanisa zaidi. Kuacha Jesuit
Fathers wanaofanya kazi nzuri, naona bado taasisi zingine za kidini
zina nafasi kubwa sana ya kuangazia fursa mbali mbali zaidi ya ibada, nina jua
kuna baadhi ya taasisi zimejikita hasa katika kutoa huduma za kielimu na afya
(pongezi kwao kwa kazi nzuri), lakini vipi kuhusu zingine kama tafiti na
uwekezaji katika teknolojia na huduma zinazo ijenga jamii na kulinda mazingira.
Nimeona jinsi imani
inavyo tuunganisha sote na kuwa kitu kimoja. Ina ufanya tuwe ndugu na kuhuisha
nafsi zetu kwa njia ya kipekee, inatufanya kuwa binadamu bora na kukwepa maovu.
Licha ya hayo yote, kama kila siku ya ibada watu watatoka wakiwa na mistari
mipya ya neno la Mungu na wakiwa na imani ya kuina paradiso naona tutakuwa bado
hatuitendea kazi rasilimali tuliyonayo ambayo ni umoja wa waumini. Hakuna jambo
gumu kama kuwaweka watu pamoja sehemu moja na kuwapa maarifa, naamini kabisa
makanisa yetu yanaweza fanya zaidi ya kutoa mapepo na kutabiria watu utajiri.
Maana dunia inabadilika kila siku, maarifa yanazidi potea na kupotoshwa na wale wasiotaka ona watu wakifunguka kifikra, hivyo basi kila rasilimali (watu, makanisa, maarifa ya waumini/viongozi, michango/sadaka) iliyopo mbele yetu
inatakiwa tumika kusaidia sukuma gurudumu la maendeleo mbele kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla na si imani husika, kwa kweli naona makanisa yetu
bado hayajafanya kazi kubwa sana kulifanya hili kuwa uhalisia.

Comments
Post a Comment